Watanzania wapo katika sintofahamu wakijiuliza maswali mengi kama bajeti itakuwa ni Balaa au tunu? Hali hii, inatokana na ukweli kwamba bajeti ya mwaka 2011/2012, imemalizika, huku kukiwa na utekelezaji duni katika baadhi ya maeneo.
Kwa mfano wa bajeti ya Wizara ya Uchukuzi, iliongezewa fedha katika sekta ya usafiri wa meli, ambapo ilitengewa Sh bilioni 9, lakini hadi mwaka unamalizika Serikali ilikuwa haijapeleka fedha ilizoahidi katika bajeti hiyo. Akiwasilisha mwelekeo wa bajeti ya 2012/13 mbele ya Kamati ya Fedha na Uchumi, Dar es Salaam wiki iliyopita, Waziri wa Fedha, Dk Mgimwa, alisema inatarajiwa kuwa Sh trilioni 15, ikilinganishwa na Sh trilioni 13.5 za mwaka 2011/12.
Alisema bajeti hiyo, imeweka vipaumbele saba, kipaumbele cha kwanza kikiwa ni miundombinu.Miundombinu imegawanyika katika makundi manne ya reli, umeme, maji salama, usafirishaji na uchukuzi ambavyo vimetengewa Sh trilioni 4.5. Vipaumbele vingine katika bajeti hiyo ni kilimo, viwanda, rasilimali watu, huduma za jamii, utalii, biashara ya ndani na nje na huduma za fedhaHata hivyo, taarifa za ndani zinaeleza kuwa fedha zilizopelekwa katika Wizara ya Uchukuzi kwa ajili ya miradi ya maendeleo ni Sh bilioni 252, huku sekta ya usafiri wa reli ikitengewa matumizi ya Sh bilioni 130.