POLISI mkoani hapa imempa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) saa 12 kujisalimisha vinginevyo adhalilishwe. Polisi pia inashikilia viongozi watatu wa juu wa Chadema, akiwamo Mwenyeki wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavita), John Heche, kwa tuhuma za kutoa lugha za uchochezi na ukabila kwa Rais na wananchi wake.
Habari za kipolisi zinadai kuwa wengine waliokamatwa ni Nelson Mawazo ambaye alikuwa Diwani wa Sombetini (CCM) ambaye hivi karibuni alihama chama hicho pamoja na Mwenyekiti wa zamani wa UVCCM wa Wilaya ya Arusha, Ally Bananga na kujiunga Chadema hivi karibuni.
Naibu Kamishina wa Jeshi la Polisi nchini, Isaya Mngulu alipoulizwa juu ya hao kukamatwa hakukanusha wala kuthibitisha, bali alisema wanahojiwa kwa maneno waliyotoa kwenye mkutano wa hadhara Jumamosi. ‘’Kweli kuna viongozi wa Chadema tumewakamata baada ya maneno waliyotoa katika mkutano wa hadhara Jumamosi, lakini kwa sasa ni mapema kuyataja,’’ alisema Mngulu.
Hata hivyo, Naibu Kamishina huyo alisema Polisi inamtaka Mbunge huyo ajisalimishe kabla ya saa 12 jioni (juzi) baada ya jitihada za makusudi za kuheshimiana kushindikana ili aende Polisi mwenyewe. Mngulu alisema si kwamba Polisi inashindwa kumpata, bali inampa muda na iwapo utapita bila kujisalimisha, hatua kali za kumsaka zitafanyika na hiyo haitatambua ubunge wake, kwani hayuko juu ya sheria za nchi. ‘’Nassari njoo mwenyewe Polisi vinginevyo itakudhalilisha na haitautambua ubunge wako, kwani wewe hauko juu ya sheria,’’ alisema.
Naibu Kamishina huyo alisema katika mkutano wa hadhara Jumamosi uliohudhuriwa na viongozi kadhaa wa Chadema akiwamo Mwenyekiti Freeman Mbowe,
matamshi ya uchochezi yalitamkwa. Alisema miongoni mwa matamshi hayo ni
- ‘’kumpiga marufuku Rais wa Nchi, Jakaya Kikwete, kukanyaga jimbo la Arumeru Mashariki na Kanda ya Ziwa, kwani maeneo hayo ni ya Chadema’’.
- Mngulu alitaja matamshi mengine ambayo yanamdhalilisha Rais na mwanawe, Ridhiwani, yakihusisha uteuzi anaoufanya Rais kwa viongozi mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment